Michezo Bayern yakaribia kutawazwa mabingwa mara nne mfululizo
Bayern Munich yafungua mwanya wa pointi saba kileleni mwa ligi ya Ujerumani Bundesliga, Borussia Dortmund nayo yatoshana nguvu na watani ...

http://clemencekarani.blogspot.com/2016/04/michezo-bayern-yakaribia-kutawazwa.html
Bayern Munich yafungua mwanya wa pointi saba kileleni mwa ligi ya
Ujerumani Bundesliga, Borussia Dortmund nayo yatoshana nguvu na watani
wao wa jadi Schalke 04 na kutoa mwanya kwa Bayern kutangaza ubingwa na
mapema.
Bayern Munich imesogea karibu na ubingwa wake wa nne mfululizo katika
Bundesliga baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya VFB Stuttgart siku ya
Jumamosi na kufungua mwanya wa pointi saba wakati ikibakia michezo
mitano hadi mwisho wa ligi.Borussia Dortmund inayoshikilia nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, iliridhika na sare ya mabao 2-2 dhidi ya watani wa jadi Schalke 04 jana Jumapili wakati Hertha BSC Berlin , iliyoko katika nafasi ya tatu ilitoshana nguvu na Hannover iliyoko mkiani mwa ligi kwa mabao 2-2.
Nikitakiwa kuchagua kati ya ushindi wa mchezo wa watani wa jadi Derby na kufikia nusu fainali ya kombe la Uropa ligi , nitapenda kusonga mbele katika Europa League, amesema kocha wa BVB Thomas Tuchel katika mahojiano na kituo cha Sky kabla ya mchezo huo wa watani wa jadi.
BVB yawaweka nje wachezaji wake wa kikosi cha kwanza
Wachezaji wa kikosi cha kwanza wanane waliachwa nje na kocha huyo wa BVB katika mchezo huo muhimu wa watani wa jadi , siku nne kabla ya mchezo mwingine muhimu wa marudiano na FC Liverpool katika Europa League. Nisingependa kuhatarisha wachezaji wangu kuumia kutokana na hali ya michezo mingi muhimu msimu huu, amesema kocha Thomas Tuchel.
Katika mchezo wa jana ambao ulikuwa na kila hali ya ushindani na purukushani za uwanjani Tuchel ametoa tathmini ya katikati.
"Naridhika na jinsi tulivyocheza, lakini sijaridhika na mabao mawili tuliyofungwa. Baada ya bao la kusawazisha 2-2 tulipata nafasi nyingi za kuweza kupata mabao na katika kipindi cha kwanza pia tulipata nafasi nyingi, za kupata bao la kuongoza. Ndio sababu nahisi kulikuwa na uwezekano wa kupata ushindi. Lakini kwa hakika, kwa sare ya bao 2-2 hapa siwezi kulalamika."
Jana lilikuwapo pia pambano lingine la watani wa jadi kati ya FC Koln na Leverkusen. Leverkusen iliibuka jioni ya jana kidedea baada ya kuishinda FC Koln kwa mabao 2-0. Hata hivyo mchezo huo ulikuwa na hamasa tele na ukamalizika kwa timu zote kuwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya mlinzi wa kushoto Wendel wa Leverkusen na Beaterncuop wa FC Kolon kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Huyu hapa mlinda mlango wa Leverkusen Bernd Leno.
"Nadhani kila mtu amehisi kwamba hamasa ilikuwa kwa kiasi fulani juu mno, hata katika baadhi ya mapambano uwanjani. Tulitambua , kwamba tulipaswa kujiweka vizuri uwanjani, kwasababu wapinzani wameangukia pua. Ndio sababu ulikuwa ushindi muhimu sana. Lakini tunatambua pia, kwamba hatukucheza vizuri sana. Mara kadhaa tulitetereka na haukuwa mchezo sahihi kwetu. Lakini naamini kwamba muhimu ni kuwa tumeshinda, na kutia kibindoni pointi na muhimu zaidi hatukufungwa bao. Hii inatupa hali ya kujiamini zaidi kwa ajili ya michezo mitano ijayo."
Homa ya kushuka daraja yapanda Bundesliga
Homa ya kushuka daraja inazikumba timu karibu saba katika Bundesliga. TSG Hoffenheim ambayo mwezi mmoja uliopita ilikuwa katika nafasi ya moja kwa moja kushuka daraja imebadilisha majaaliwa yake na inamatumaini ya kubakia katika daraja la juu iwapo itafanya vizuri katika michezo yake mitano ijayo. Hoffenheim iko katika nafasi ya 14 hivi sasa baada ya mwishoni mwa juma kuizaba Eintracht Frankfurt kwa mabao 2-0 ikiwa ugenini.
Werder Bremen ambayo inaikabili Borussia Dortmund wiki ijayo imo katika hali mbaya ya kushuka daraja kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuporomoka hadi nafasi ya 16 baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Augsburg , timu nyingine iliyoko katika hatari ya kushuka daraja.
Augsburg haijajinasua kutoka katika hatari hiyo licha ya kupanda hadi nafasi ya 14 , ikiwa na poimti 31 mbili tu nyuma ya Werder Bremen yenye pointi 28.
Hannover licha ya kutoka sare na Hertha Berlin ya mabao 2-2 inashikilia mkia ikiwa na pointi 18 na itakuwa miujiza iwapo itatoka katika janga hilo msimu huu.
Ingolstadt timu iliyopanda daraja msimu huu imejihakikishia pointi za kuibakisha katika daraja la juu baada ya kuiangusha Borussia Moengchengladbach kwa bao 1-0 nyumbani ,na kutibua mipango ya Gladbach kucheza katika Champions League msimu ujao.
Leicester City hawashikiki
Na katika premier League nchini Uingereza , meneja wa viongozi wa ligi hiyo Leicester City Claudio Ranieri alibubujikwa na machozi baada ya kufurahishwa na vijana wake walipoitandika Sunderland kwa mabao 2-0 na kuongeza uwezekano wa timu hiyo kutawazwa mabingwa wa Premier League kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo, baada ya kufungua mwanya wa pointi 7.
Alikuwa Jamie Vardy aliyeipa ushindi Leicester kwa kupachika mabao mawili muhimu jana Jumapili.
Na Tottenham Hotspurs iliyoko katika nafasi ya pili ilipachika mabao matatu dhidi ya Manchester United jana Jumapili, kipigo ambacho kina maana Leicester imejihakikishia kuwamo katika timu nne za juu ambazo zitashiriki katika michezo ya Champions League msimu ujao.
Kocha wa Manchester United Louis van Gaal amesema kwamba hajutii kutochukua kazi ya kuifunza Tottenham Hotspurs baada ya timu hiyo ya mjini London kuchafua matumaini ya timu yake kucheza katika Champions League jana.
Arsenal nayo imepoteza mwelekeo baada ya kulazimisha sare ya mabao 3-3 dhidi ya West Ham United siku ya Jumamosi.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp anaamini kijana chipukizi Divock Origi yumo mwanzoni mwa kitu muhimu baada ya kupachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Stoke City jana Jumapili.
Klopp anahisi Origi ataimarika siku hadi siku, akisema yuko katika njia nzuri , na hii ni msingi mzuri na sasa watafanyakazi kwa pamoja kufikia lengo lake.
Barcelona yateleza katika La Liga
Katika La Liga nchini Uhispania Barcelona iliteleza tena wiki hii na kupunguza mwanya wa pointi kileleni hadi pointi tatu baada ya kugaragazwa kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad.
Atletico Madrid na Real Madrid sasa zinainyemelea Barcelona zikitengana kwa pointi tatu na nne kwa Real.
Real Madrid iliirarua Eibar kwa mabao 4-0 na Atletico Madrid iliizaba Espanyol kwa mabao 3-1.
Duru ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika
Katika ligi ya mabingwa barani Afrika Enyimba ya Nigeria iliikandika Etoile Sahil ya Tunisia kwa mabao 3-0 nyumbani jana Jumapili katika mchezo wav kwanza wa timu 16 bora barani Afrika. Ushindi huo umeiweka Enyimba mabingwa mara mbili wa Afrika katika ukingo wa kufuzu kuingia katika awamu ya makundi ya kinyang'anyiro hicho cha mabingwa wa Afrika.
Mabingwa mara nane wa kombe hilo la Afrika El Ahly ya Misri ilitoka suluhu ya bao 1-1 na mabingwa wa Tanzania Yanga ya mjini Dar Es Salaam , wakati Zamalek ya Misri ilishinda mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Mouloudia Bejaia ya Algeria.
Zesco United ya Zambia iliwashangaza wenyeji wao Stade Malien ya Mali kwa kuichapa mabao 3-1 na ASEC Mimosas ya Cote d'Ivoire ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya. Al Merrickh ya Sudan ilipata nayo sare ya mabao 2-2 dhidi ya mabingwa wa mwaka 2014 Entente Setif ya Algeria.
Katika kombe la shirikisho Azam ya Tanzania iliionja raha ya ushindi pale ilipoizaba Esperance ya Tunisia kwa mabao 2-1. Villa ya Uganda licha ya kupatiwa fedha za gharama ya safari kwenda Morocco na rais Yoweri Museveni ilitumbukia katika kikaango na kuduwazwa na FUS Rabat kwa mabao 7-0.
Ligi ya mabingwa Ulaya, Ni "Vita Santiago Bernabeu".
Na katika ligi ya mabingwa barani Ulaya , kesho katika uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid kutawaka moto, wakati Real Madrid iliyoduwazwa na VFL Wolfsburg ya Ujerumani wiki iliyopita kwa kucharazwa mabao 2-0, katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Champions League barani Ulaya ambapo timu hiyo ya mjini Madrid itajaribu kulinda hadhi yake na kufikia katika duru ya nusu fainali ya Champions League barani Ulaya.
Kesho itakuwa kama vita, tukiungwa mkono na mashabiki wetu 80,000 , tutajaribu kuwavuruga Wolfsburg ," amesema mlinzi Dani Carvajal. Tutacheza kufa na kupona na nyuma yetu tukiwa na watu 80,000 wakitusapoti," ameongeza winga Lucas Vazquez.
Mshambuliaji wa Real Cristiano Ronaldo ameiambia tovuti ya klabu hiyo: " Tunahitaji mioyo migumu na kucheza kwa utulivu na kujua jinsi ya kuteseka. Kusonga mbele ni lengo letu kuu, ni kitu pekee ambacho kitawafanya wachezaji na mashabiki kuondoka uwanjani wakiwa na furaha.
Mchezo mwingine mgumu kesho wa mkondo wa pili wa robo fainali ni kati ya Manchester City na PSG ya Ufaransa.
Bayern Munich inacheza Jumatano ikipambana na Benfica Lisbon , hali inayoiweka Bayern katika wasi wasi baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 mjini Munich wiki iliyopita, na Barcelona inasafiri kwenda mjini Madrid kupambana na Atletico Madrid katika mchezo mwingine wenye sura ya vita mjini humo, baada ya Barca kupata ushindi mwembamba pia wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico.
FIFA kukagua viwanja vya kombe la dunia Urusi
Siku kumi za ziara ya ukaguzi wa ujumbe wa FIFA katika viwanja vitakavyofanyiwa fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi inaanza kesho mjini St. Petersburg, moja kati ya miji 11 nchini humo itakayokuwa mwenyeji wa kombe la dunia, linaripoti shirika la habari la Tass. Mbali na ziara katika mji wa pili kwa ukubwa wa St. Petersburg , wajumbe watazuru miji ya Nizhny, Novgorov, Volgograd, samara, Yekaterinburg na Sochi kabla ya Aprili 14.
Riadha. Kenya kutii amri ya WADA
Kenya itatimiza muda wa mwisho wa mwezi Mei kufuata mfumo wa shirika linalopambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, Doping , WADA na kuepuka vikwazo ambavyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Rio , rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema leo Jumatatu(11.04.2016).
Akizungumza katika hafla ya chai ya asubuhi aliyowaandalia wanariadha watakaoshiriki katika mbio ndefu, marathon na mbio za dunia za nusu marathon ikulu mjini Nairobi, Kenyatta amesema serikali yake imeupa mswada huo umuhimu na anaufuatilia kwa karibu.
Ifikapo mwishoni mwa juma, mswada wa kupambana na madawa hayo, utakuwa umepitishwa na bunge na nitautia saini kuwa sheria ili kusiwe na kisingizio cha kuinyima timu yetu kushiriki katika michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro mwezi Agusti, amesema.
"Tunafahamu kuna watu wanaotafuta visingizio kuhakikisha kwamba Kenya haishiriki katika Olimpiki.
Hatutawapa nafasi hiyo" alinukuliwa akisema katika taarifa rasmi ya serikali.
Kenya imepatiwa muda wa nyongeza wa mwezi mmoja hadi Aprili 7 kufuata mfumo wa WADA ama itakabiliwa na vikwazo ambavyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka huu.
Infantino ajitetea
Rais wa FIFA Gianni Infantino ameelezea ripoti za vyombo vya habari kuhusu mkataba wa Televisheni ambao umeibuka katika nyaraka za siri za Panama zilizovuja kuwa zinatia aibu. Infantino, aliyechaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho hilo la vyama vya kandanda duniani mwezi Februari , ameliambia gazeti la Kicker la Ujerumani katika mahojiano yaliyochapishwa leo Jumatatu (11.04.2016) kuwa mkataba huo wa televisheni aliutia saini kama mkurugenzi wa sheria wa shirikisho la kandanda la Ulaya UEFA , ulikuwa juu ya chombo hicho.
Raia huyo wa Uswisi mwenye umri wa miaka 46, katibu mkuu wa zamani wa UEFA , amesema anaukaribisha na hana wasi wasi kabisa na uchunguzi unaofanywa na maafisa wa ofisi ya mwendesha mashitaka ya Uswisi.
Ugunduzi katika kile kinachojulikana kama Nyaraka za Panama unaonesha kwamba Infantino alitia saini mkataba huo kuhusu haki za kuonesha michuano ya Champions League katika TV pamoja na kampuni inayomilikiwa na ndugu kutoka Argentina Hugo na Mariano Jinks, ambao wameshitakiwa nchini Marekani mwezi Mei katika uchunguzi wa ulaji rushwa.
Lakini Infantino ameliambia gazeti la Kicker utoaji wa haki hizo za TV ulikuwa sahihi na kuelezwa kwa makini na haki hizo zilipitia katika utaratibu wa tenda.
Werder Bremen yamng'ang'ania kocha wake Skripnik
Viktor Skripnik atabakia kuwa kocha wa Werder Bremen licha ya kuporomoka hadi katika eneo la hatari katika msimamo wa ligi ya Bundesliga , amesema meneja mkuu Thomas Eichin leo Jumatatu(11.04.2016).
"Nimetathmini hali na kuangalia Viktor yuko imara kiasi gani.
Wote tunahisia kuwa ni imara kwa kiasi cha kutosha," Eichin amesema.
Eichin ameongeza hajafanya mazungumzo na makocha wengine baada ya Bremen kuporomoka katika robo ya mwisho ya eneo la hatari baada ya kufungwa mabao 2-1 na Augsburg nyumbani siku ya Jumamosi.
Messi mchezaji mwenye kipato cha juu
Na mchezaji nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi amebaki kuwa mchezaji kandanda anayelipwa fedha nyingi duniani kwa mwaka akiwa na mapato ya euro milioni 74 kwa mwaka , kwa mujibu wa ripoti zinazotarajiwa kuchapishwa kesho na jarida la mchezo wa kandanda nchini Ufaransa.
Cristiano Ronald wa Real Madrid anafuatia akiwa na mapato ya euro milioni 67.4 kwa mwaka na Neymar anafuatia akiwa na mapato ya euro milioni 43 , watatu hao wakiendelea kuwa juu kwa miaka mitatu mfululizo.