Serikali ya Burundi kususia mazungumzo ya amani
Serikali ya Burundi imesema itagoma kushiriki katika mazungumzo yaliokwama kukomesha mzozo wa Burundi uliodumu kwa miezi kadhaa sasa ve...

http://clemencekarani.blogspot.com/2016/04/serikali-ya-burundi-kususia-mazungumzo.html
Serikali ya Burundi imesema itagoma kushiriki katika mazungumzo
yaliokwama kukomesha mzozo wa Burundi uliodumu kwa miezi kadhaa sasa
venginevyo shauriwe kwanza kuhusu washiriki wengine wa mazungumzo hayo.
Wakati serikali ya Marekani ikihimiza maafisa wa serikali ya Burundi
kuuzima mzozo huo wa mwaka mmoja taarifa kutoka ofisi ya rais
iliotangazwa kwenye radio ya taifa nchini Burundi hapo Jumatano na
kusikika mjini Nairobi Kenya imetowa masharti kadhaa ili serikali
ijiunge na kile kinachoitwa "mazungumzo ya Burundi."Willy Nyamwite afisa mawasiliano katika ofisi ya rais amesema serikali ya Burundi lazima ishauriwe na kwamba lazima wafikie makubaliano kuhusu watu wanaopaswa kualikwa,tarehe ya kufanyika mazungumzo hayo na mahala pa kufanyikia mazungumzo hayo.
Pia ameongeza kusema kwamba serikali inasubiri mwaliko rasmi.
Baadae ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ndio kwanza imepokea mwaliko huo wa mazunguzo ya mzozo wa Burundi yaliopangwa kufanyika Jumatatu na kwamba inauchambuwa na itajibu wakati wowote ule kwa njia zinazostahiki.
Burundi iko kwenye mfarakano wa kisiasa kwa zaidi ya mwaka mmoja ambapo watu 270,000 wamelazimika kukimbilia uhamishoni na wengine zaidi ya 500 kuuwawa.
Mkapa anaongoza mazungumzo

Kuanza upya kwa mazungumzo hayo kumekaribishwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku kama ni njia bora za kurudisha amani na utulivu kwa Warundi na kuwataka wadau wote washiriki mazungumzohayo bila ya kuweka masharti.
Lakini serikali mara kwa mara imekuwa ikigoma kuketi meza moja na kundi kuu la muungano wa upinzani CNARED na viongozi wa upinzani walioko ndani ya nchi na wale walioko uhamishoni ambao inawashutumu kwa kuchochea ghasia.
Masharti ya serikali
Nyamwite amenukuliwa akisema kwenye radio kwamba "wale walioshambulia maisha ya raia , wale waliotarajia kupinduwa taasisi za serikali ambazo zimechaguliwa kidemokrasia na wengine waliohusika na uasi wa kutumia silaha katika nchi yao hawawezi kuitwa kushiriki mazungumzo hayo."
Muungano wa upinzani wa CNARED umesema uko tayari kushiriki mazungumzo hayo ya Jumatatu juu ya kwamba bado haukupokea mwaliko rasmi.
Afisa wake wa mawasiliano Jeremie Minani ameitaka serikali ya Burundi itambuwe kwamba sio sehemu ya upatanishi bali ni sehemu ya mzozo kama ilivyo kwa muungano wa upinzani wa CNARED.
Amesema hawastahiki kuandaa orodha ya washiriki au kuweka agenda ya mazungumzo hayo. Mzozo wa sasa Burundi ulianza kufuatia uamuzi tata wa Rais Pierre Nkurunziza mwezi Aprili mwaka jana kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwezi wa Julai uliosusiwa na upinzani ambapo alishinda.